MAFUNZO KWA WAAJIRIWA WAPYA WA TLSB
Waajiriwa wapya wapatao 51 wameaswa kuzingatia Sheria, Kanuni na taratibu za Utumishi wa Umma ili kutekeleza majukumu yao ya kila siku kwa weledi na ufanisi.
Hayo yamesema tarehe 07 Mei, 2025 na Mgeni Rasmi na Mkurugenzi Mkuu wa TLSB Dkt. Mboni Ruzegea katika mafunzo kwa Waajiriwa wapya kazini (Induction training) yanayofanyika katika Ukumbi wa Mikutano ADEM - Bagamoyo, mkoani Pwani.
Akifungua mafunzo hayo, Dkt. Ruzegea amewakaribisha na kuwataka Watumishi
hao wapya katika Utumishi wa Umma kufuata Sheria, taratibu na kanuni za Utumishi wa Umma ili wasijiingize matatizoni na hatimaye kupoteza kazi zao.
"Hii ni dhamana kubwa mliyopewa na Serikali kuwatumikia wananchi, wapo vijana wengi wenye sifa kama zenu, lakini mpaka sasa bado wanatafuta ajira. Hivyo hii ni nafasi adhimu kwenu mkaitumikie kwa uaminifu na bila manung'uniko" ameeleza Dkt. Ruzegea.
Dkt. Ruzegea ameongeza kuwa, mbali na Sheria, Kanuni na taratibu katika utumishi wa umma, Waajiwa hao wanapaswa pia kusoma, kuelewa na kuzingatia Sheria ya TLSB ili kuifahamu Bodi, Majukumu yake na mawanda yake katika kutekeleza majukumu yao.
Vilevile ameongeza kuwa, mbali na sheria ya TLSB, wanapaswa kufahamu Muundo wa Bodi, kuanzia ngazi ya juu ambayo ni Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Kamishna wa Elimu, Bodi ya Wakurugenzi, Wakuu wa Idara na Vitengo mpaka ngazi za chini kabisa kwa watumishi.
Aidha, amewataka kufuata utamaduni (Organizational Culture) na thamani (Values) za TLSB ili kuishi kwa amani na kuepusha migogoro kazini.
"Kama ilivyo sehemu yeyote ile, TLSB tuna utamaduni wetu na thamani zetu ambazo zinatutofautisha na wengine, hivyo mnapaswa kuishi kwa kufuata utamaduni huo kwani TLSB ni kama Meli kubwa iliyobeba kila mtu na utamaduni wake, lakini mkishakaa ndani yake mnapaswa kuwa na utamaduni mmoja" ameongeza

